Jukwaa la kidigitali la kusambaza muziki linaoongoza Afrika, Mdundo limeendelea kufanikiwa kuongezea tasnia ya muziki thamani kwa kuwawezesha wasanii kusamabaza, kutangaza na kunufaika na muziki wao. Uwepo wa watumiaji zaidi ya milioni 38.7 kwa mwezi na utendaji unaogusa nchi za Afrika, Mdundo imeendelea kuwa mstari wa mbele ikiongoza mageuzi ya kidigitali kwenye muziki.
Mwezi wa Januari mwaka 2025, tovuti ya Mdundo ilianza majira ya ugawaji wa mirahaba ambalo ni zoezi linaloendelea, na kunufaisha haki za wadau wa muziki barani Afrika. Toka kuanzishwa kwa zoezi hili, zaidi ya wasanii laki mbili (200,000) wameweza kupokea mirahaba yao kupitia jukwaa hili na idadi ya wanufaika imeendelea kuongezeka kadri mzunguko wa malipo unapofanyika. Mafanikio haya yanadhihirisha msimamo wa Mdundo kwenye kukuza na kuimarisha soko la muziki kwa wasanii wa barani Afrika.
Martin Moller Nielsen ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mdundo, ameonesha fahari kwenye mafanikio ya jukwaa hili kwa kusema: “Lengo letu siku zote limekuwa ni kuwapa wasanii wa muziki Afrika, jukwaa imara la kukua kimuziki kwa kuendelea kuwapa kipato chao. Tumechangia kwenye kukuza wanamuziki huku tukishiriki kwenye maendeleo ya tasnia ya muziki ya Afrika kiujumla.”
Mdundo imetoa mirahaba ya kiasi cha Dola 800,000 sawa na Bilioni 2,075,200,000/-TZS kwa wasanii wa muziki Afrika, katika kipindi cha miezi sita ya mwaka 2024, yaani malipo ya mirahaba hiyo yameanza kutolewa Januari 2025 kwa mapato ya kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2024.
Bi. Phiona Nafuna ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Utoaji Leseni Mdundo, amegusia kuwa jukwaa hili ni kwaajili ya wasanii wa muziki, amesema: “Mdundo inabaki na lengo la kuwawezesha wanamuziki wa Afrika, kwa kuwahakikishia wanapata stahiki zao kwa usawa na kwa wakati. Hili ni dhumuni kuu kwenye lengo la kuwashika mkono wanamuziki, kuongeza uwanda wa tasnia ya muziki na kuchangia ukuaji wa mfumo wa kisheria na kiuchumi ndani ya tasnia hii.”
Kwa kuongeza, katalogi ya Mdundo inatajirishwa na ushirikiano na lebo kubwa za kimataifa kama Africori, Mavin, Universal Music Group, na Warner Music Group, lakini pia na viongozi wa kikanda kama Slide Digital na Content Connect Africa. Jukwaa hili linahimiza uwepo wa maudhui ya muziki ya nchi na nchi, kukiwepo aina tofauti za muziki kama Kalenjin na Kamba kutoka Kenya, Singeli kutoka Tanzania na Hausa kutoka Nigeria. Hili limewezesha kuimarisha mahusiano na wasikilizaji, kuwaongezea umaarufu wanamuziki na kutengeneza mianya mipya ya kuingiza kipato kwa wadau stahiki.
Mbeleni, Mdundo inalenga kutoa malipo ya mirahaba inayofikia Dola Milioni 1.5 hadi Milioni 2 sawa na Bilioni 3,981,000,000/- TZS hadi Bilioni 5, 188,000,000/- TZS ikifika mwaka 2026, kwa kuongeza umakini maalumu kwenye kukuza wanamuziki wa ndani na kuonesha vipaji vyao ulimwenguni kote. Kadri Mdundo inavyoendelea kupanuka, ari yake ya kushika mkono wanamuziki wa Afrika inabaki imara zaidi, kwa kuhakikisha inafungua njia kwa wasanii kukua kwenye soko la muziki la kimataifa.